Wednesday 24th, April 2024
@Shule ya Msingi Kambubu
Tarehe 23/6/2017 ni Siku ya Mtoto wa Afrika ambapo Dr. Charles Mlingwa, Mkuu wa Mkoa wa Mara anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika kuadhimisha siku hiyo katika ngazi ya Mkoa. Maadhimisho haya ni katika kutekeleza azimio lililopitishwa na Nchi 51 za Umoja wa Afrika mwaka 1990 likiwa na kauli mbiu ya "Maendeleo Endelevu 2030: Imarisha Ulinzi na Fursa sawa kwa Watoto". Hafla hii itafanyika katika shule ya Msingi Kambubu, Kijiji cha Kambubu, Kata ya Nyamang'uta, Wilaya ya Bunda. Siku hii ya Mtoto wa Afrika itaadhimishwa katika shule hii kwa sababu ya mchango wake mkubwa katika kutambua, kuthamini na kumshirikisha mtoto katika kumjengea tabia ya kujitegemea kama vile kutunza bustani ya mbogamboga, kushirikiana na wazazi katika kuhakikisha kuwa mtoto anapata chakula awapo shuleni, kuhamasisha wadau wengine wa maendeleo kutoa michango ya hali na mali ili kufanikisha azma ya kumsaidia mtoto awe na mazingira muhimu ya kusoma na hivyo aweze kutimiza malengo yake.
Wadau tajwa wa Maendeleo waliohusika katika kuiongezea serikali nguvu kumsaidia mtoto huyo ni pamoja na Mashirika ya PCI-Tanzania, Compassion na Zawadi Zinduka. Pamoja na masuala mengine, Wadau hawa wanaisaidia Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali kama vile: Kuboresha miundombinu mashuleni, kuzuia ukatili dhidi ya Watoto kama vile kupewa mimba, vipigo, ubakaji, ndoa za utotoni, ajira za utotoni na migogoro ya ndoa ambayo hupelekea watoto kukosa haki zao za msingi katika familia.
Ili kuondoa changamoto hizo, Wilaya ya Bunda kama mwakilishi wa Wilaya zingine Mkoani Mara na Taifa kwa ujumla, imedhamiria kutekeleza mikakati kadhaa ikiwemo kuhamasisha jamii katika ujenzi wa miundombinu mashuleni, kutoa elimu kwa jamii kuacha ukatili dhidi ya watoto ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua kali watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo na kuelimisha jamii katika kutoa elimu ya makuzi na stadi za maisha kwa watoto wote.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0754821313
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda