Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mh. Dr. Vicent Anney amefanya mkutano wa hadhara na Wanakijiji cha Karukekere, Kata ya Namuhula katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa kusikiliza kero na changamoto wanazokabiliana nazo.
Mkuu wa Wilaya alikutana na Wanakijiji hao alipokuwa akifanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali katika Kijiji hicho siku ya tarehe 23/10/2023.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Karukekere Bw. Daniel Peter Ngawa, alimshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kuja kuwatembelea na kukagua miradi mbalimbali waliyonayo katika Kijiji chao, pia alimueleza changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo miundombinu ya Barabara kutokuwa rafiki hasa wakati wa mvua, njia kushindwa kupitika kutokana na ubovu wa Barabara na kukatika kwa madaraja, hivyo kupelekea shughuli nyingi za kiuchumi kukwama.
Bw. Ngawa alisema mbali na changamoto wanazokabiliana nazo, Kijiji kimeweza kuchangia kiasi cha Tshs Milioni 20 ya mapato yao katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kutokana na zao la Dengu kwa mwaka 2023.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya alianza kwa kusema, changamoto kubwa aliyoiona ni wananchi wengi kutokuwa na vyoo, hivyo alimuagiza Mtendaji wa Kijiji pamoja na vitongoji kushirikiana kwa pamoja katika kusimamia masuala ya uchimbaji wa vyoo katika kaya ili kukabiliana na milipuko ya magonjwa.
Alimuagiza Mtendaji wa Kijiji kuanzia siku ya Jumatatu tarehe 30/10/2023 ahakikishe wanapita kwenye kila kaya na kukagua watu wasiokuwa na vyoo na kuanza kuwachukulia hatua ikiwemo kuwatoza faini.
Mh. Dr. Anney alisema, changamoto nyingine aliyoiona kwenye Kijiji chao ni Watoto wengi kutokupelekwa shuleni hadi umri wa kuanza shule kupita, hivyo alimuagiza Mtendaji wa Kijiji kuhakikisha wanashirikiana na viongozi waliopo kwenye vitongoji kwa kupata takwimu sahihi na kuandikisha Watoto wote walio na umri wa kupelekwa shule lakini wapo nyumbani wahakikishe wanahudhuria shuleni na kuanza masomo mara moja.
Mkuu wa Wilaya alisema, suala la Barabara ameshamuagiza Meneja TARURA kuhakikisha anatatua changamoto hizo ili kuhakikisha barabara zinapitika kipindi chote kwa mwaka mzima. Pia alimuagiza Meneja TANESCO kuhakikisha wanaweka kwenye bajeti yao ya mwaka huu suala la kuwaletea umeme Wanakijiji pamoja na eneo la Mradi wa Maji ambao unatumia jenereta katika shughuli zake hivo kupelekea gharama za uzalishaji kuwa kubwa mno.
Mh. Dr. Anney aliwapongeza Wanakijiji na Viongozi wa Chama kwa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi vizuri kwa kuhakikisha suala la elimu katika Kijiji chao wanalipa kipaumbele katika Ujenzi wa shule za Msingi na Sekondari kwa ajili ya kuhakikisha Watoto wao wanapata elimu iliyo bora na ya uhakika.
Pia aliwapongeza kwa Ujenzi wa Jengo la kinamama la kujifungulia katika Zahanati ya Karukekere walilolijenga kwa nguvu ya wananchi, hivyo aliwaahidi kuwachangia kiasi cha Tshs Milioni Moja ili kukamilisha Ujenzi huo.
Mkuu wa Wilaya aliwaagiza Wanakijiji kwa mwaka huu kuhakikisha wanapanda zao la Mtama na Pamba kwa ajili ya kujiongezea mapato katika Kijiji chao, na kuwaasa kuacha tabia ya kuchanganya zao la Pamba na Mahindi katika shamba moja kwani ni hatari sana, hii ni kutokana na dawa zinazopuliziwa kwenye Pamba kuwa ni kali na hatari kwa Afya ndio maana aliwaasa kuacha tabia ya kuchanganya mazao hayo pamoja wakati wa upandaji.
Mh. Dr. Anney alimuagiza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bw. Oscar Jeremiah Nchemwa, kuhakikisha mbolea inaletwa katika Kijiji chao. Pia aliwaomba Wanakijiji kutunza Ulinzi na usalama.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0754335739
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda