*VIKUNDI VYA WATU WENYE ULEMAVU, WANAWAKE NA VIJANA VYAPATIWA MAFUNZO.*
Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii imeendesha mafunzo ya mikopo isiyo na riba kwa vikundi vitakavyonufaika na mkopo huo ikiwa sambamba na Elimu ya ujazaji wa fomu za mikataba. Mafunzo hayo yametolewa Aprili 9, 2020 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Bunda.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Bi.Beatrice Gwamagobe amesema mjasiriamali lazima awe Mbunifu ili kukuza na kuongeza thamani biashara anayoifanya.
”Tunategemea kama mkulima wa mpunga utakoboa utapata mchele na utauza pumba.”
Amevitaka vikundi vyote vitakavyonufaika na mkopo vihakikishe vinatumia fedha hizo kuendeleza ujasiriamali ili kuepuka usumbufu wakati wa marejesho huku akisisitiza kuwa wabunifu wa mbinu mbalimbali zitakazo wawezesha kutoka hatua moja kimaendeleo kwenda nyingine.
“Ni wakati wa vikundi kufanya kazi kwa ushirikiano na kuongeza ubunifu ili kuleta matokeo chanya katika kujikwamua kiuchumi na kutengeneza ajira kwa wengine.”
Kwa upande wake, Afisa Maendele ya Jamii Msaidizi Bi. Liliani Mugwe ametoa rai kwa wanavikundi kufuata taratibu za kifedha kwa kufanya marejesho kwa wakati.
"kila mwanakikundi anawajibu wa kufuata taratibu za kurejesha mkopo. Hiyo itasaidia kujenga uaminifu na kusaidia kufikisha malengo ya kikundi. Mkumbuke baada ya kupata slip ya benki mnaleta ofisini hapa kwa ajili ya kupata uthibitisho kuwa marejesho yamepokelewa.” Amesema Liliani
Naye, Afisa vijana, Colmani Mushi amewataka wanavikundi hao kutumia fedha hizo kulingana na lengo.
" Baada ya miezi mitatu tunategemea kila kikundi kitafanya marejesho ya mkopo. Ninyi viongozi mkasimamie hizi pesa. Tunategemea wote mtafanya vizuri ili kukuza kipato. kwa wakulima wa bustani kama mtapata nafasi mkatembelee Bulamba farmers wanajishughulisha na kilimo cha bustani na wanafanya vizuri sana”. Amesema Mushi.
Nao wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na na Dkr. John Pombe Magufuli kwa kuendelea kuwajali na kuwawezesha wajasiriamali wadogo wadogo kwa kuwapatia mkopo usio na riba na wameahidi kutumia mkopo huo kwa lengo la kukuza shughuli zao za ujasiriamali na kutimiza lengo la serikali la kuwakwamua Wajasiriamali kiuchumi.
Kwa Mwaka wa fedha 2019/2020 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda imetoa kiasi Cha shilingi milioni20 kwa vikundi vya wanawake,watu wenye ulemavu na Vijana kwa awamu hii ya pili Halmashauri inatarajia kutoa jumla ya shilingi milioni 30 kwa vikundi 13 ikiwa vikundi 3 vya walemavu, vitano vya vijana na 5 kwa wanawake. Mikopo hiyo inatolewa kwa mujibu wa sheria na miongozo inayoelekeza Mapato ya ndani ya Halmashauri kutolewa mkopo isiyokua na riba kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0754335739
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda