Halmashauri ya Wilaya ya Bunda imeadhimisha siku ya hedhi Salama Duniani, ambapo maadhimisho yamefanyika siku ya tarehe 30/5/2025 katika kituo cha Afya Ikizu. Na mgeni rasmi alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Ndugu Oscar J. Nchemwa.
Maadhimisho ya siku ya hedhi Salama Duniani huadhimishwa Kila tarehe 28/5 ya Kila mwaka, na mwaka 2025 maadhimisho yalibeba kauli mbiu isemayo: " WEZESHA MAZINGIRA YA HEDHI SALAMA YENYE UTU KWA WASICHANA NA WANAWAKE WOTE."
Mratibu wa huduma za Afya na mtoto wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bi. Elizabeth Boniface alisema, katika kuadhimisha siku hii ya Leo wameshiriki katika shughuli mbalimbali ambazo ni kutoa elimu juu ya hedhi Salama katika shule za Chisorya, Makongoro, Esperanto, Mihingo, Chamriho na Mariwanda ambapo jumla ya wanafunzi 566 walipata elimu.
Bi. Boniface alisema, mada ambazo walizifundisha kwa wanafunzi hao ni mabadiliko yanayojitokeza Kila awamu ya mzunguko wa hedhi na usafi wakati wa hedhi.
" Shule zote zina walimu wa Afya ambao wanashirikiana na wataalamu wa huduma za Afya katika kutoa elimu juu ya Afya ya uzazi na Kuna baadhi ya shule wamekuwa wakitoa taulo za kike shuleni. Pia, wamekuwa na huduma rafiki kwa vijana ambazo zimeimarishwa katika ngazi za jamii, Kila kata kumekuwa na kijana Mmoja ambaye amekuwa ni muelimisha rika katika elimu ya hedhi Salama kuhakikisha inafika ngazi za jamii." Alisema.
Ndugu Nchemwa alisisitiza kuhakikisha elimu ya Afya inaendelea kutolewa kwa vijana rika balehe ili waweze kuwa na elimu ya kutosha ya namna ya kukabiliana na madiliko ya hedhi Kila mara, na pia kuwa wasafi muda wote pale wanapokuwa katika kipindi cha hedhi kwani kitawasaidia kuepukana na magonjwa ya U.T.I na kuumwa tumbo kutoka na kutokuwa wasafi.
Sasa hivi shule zote katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda zimetengeneza eneo maalumu kwa ajili ya wasichana kuweza kujihifadhi wakati wa kipindi cha hedhi, na pia Kila shule kuhakikisha inakuwa na maji Salama ili waweze kujisafisha muda wote.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika:
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda