Katibu tawala wa Wilaya ya Bunda, Ndugu Salum Mtelela kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mh. Aswege Kaminyoge aliongoza kikao cha kamati ya lishe ngazi ya Wilaya kilichofanyika siku ya tarehe 21/11/2025 katika ukumbi wa Halmashauri uliopo Kibara Stoo.


Ndugu Mtelela aliwaagiza watendaji wa kata kuendelea kuhamasisha na kutoa elimu kwa jamii hasa wazazi kuona umuhimu wa kuchangia chakula shuleni, kwani ajenda ya chakula shuleni ni muhimu na ni suala la Kitaifa, hivyo, Kila mzazi anawajibu wa kuhakikisha anachangiwa chakula shuleni na watoto wote wanapaswa kupata mlo kamili kuanzia darasa la awali hadi Sekondari.

Katika kikao hicho Maafisa lishe wa Halmashauri zote mbili waliweza kuwasilisha kadi alama tatu ambazo zinaonyesha muelekeo wa utoaji wa chakula shuleni na kwenye jamii, kuanzia ngazi ya kata, chama hadi Halmashauri, ambapo ilionekana kwa kiasi kikubwa kumekuwepo na wimbi la watoto wanaozaliwa chini ya uzito kamili hii ni kutokana na wazazi wengine kutokula mlo kamili na kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa Afya pale wanapokuwa wajawazito.


Katika kikao hivo, mjumbe Mmoja aliwashauri watendaji wa kata kuhakikisha wanatembelea shuleni mara kwa mara ili kubaini changamoto wanazopitia walimu katika uhifadhi wa mazao shuleni baada ya kuvuna Toka shambani ama wanapoletewa na wazazi na kuweza kutatua mara Moja.

Pia, mjumbe mwingine alishauri suala la lishe liwe ni ajenda muhimu na kuu katika Kila vikao watakavyokaa na wananchi, hii itasaidia kuhamasisha uchangiaji wa chakula shuleni na wananchi kuona umuhimu wa watoto kupata lishe shuleni.

Watendaji walishauriwa kuhakikisha wanawashirikisha Maafisa tarafa na maafisa lishe ili waweze kusaidia katika kuweka msisitizo na hamasa ya kuchangia chakula shuleni.

Ndugu Mtelela alisema, tushirikane kwa pamoja katika kuhakikisha ajenda hii ya lishe inatekelezwa kwa usahihi kwa kuhakikisha wanafunzi wote wanakula chakula shuleni kuanzia darasa la awali hadi Sekondari.

Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika:
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda