Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mh. Aswege Enock Kaminyoge siku ya tarehe 1/7/2025 alifungua kikao cha Baraza la wafanyabiashara, kilichofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Kikao hicho,kilihudhuriwa na wafanyabiashara mbalimbali kutoka katika Wilaya ya Bunda, wakuu wa taasisi za umma na binafsi, wakuu wa divisheni na vitengo kutoka Halmashauri zote mbili, pamoja na kamati ya usalama ya Wilaya.
Lengo la kuitisha kikao hicho ni kuelezea fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana katika Wilaya ya Bunda,ambapo wafanyabiashara walielezea changamoto wanazokabiliana nazo katika uwekezaji wao ikiwemo kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusiana na mfumo wa uuzaji na ununuzi wa mazao kupitia stakabadhi ghalani.
Kutokana na kutokuwa na elimu hiyo wameshindwa kuelewa ni namna Gani mfumo huo unavyowanufaisha wakulima katika uuzaji wa mazao yao baada ya kuvuna kutoka shambani.
Changamoto nyingine waliyobainisha ni kutokutangazwa kwa sekta za utalii katika Wilaya ambapo walisema kama wangepata elimu ya kutosha katika sekta hizo muhimu wawekezaji wengi wangeweza kunufaika nazo.
Mh.Kaminyoge alimuagiza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda , Ndugu Stafa Nashon kuhakikisha wanaenda kuitisha kikao cha wafanyabiashara wote na AMCOS zote zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na kuhakikisha wanawapa elimu ya kutosha juu ya mfumo wa uuzaji na ununuaji wa mazao kupitia stakabadhi ghalani kabla ya msimu mwingine wa mnada wa uuzaji wa mazao hayo haujaanza.
" Halmashauri zote mbili zihakikishe zinatumia tovuti na mitandao ya kijamii kuhakikisha wanatoa elimu na matangazo ya fursa za uwekezaji ndani ya Wilaya." Alisema.
Naye, Meneja wa TRA Wilaya aliwashukuru na kuwapongeza, wafanyabiashara wote wa Bunda kwa kuweza kulipia Kodi kwa wakati hadi kupelekea mamlaka ya Kodi Wilaya ya Bunda kuvuka lengo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo mamlaka iliweka lengo la kukusanya Tshs Million 810, lakini kutokana na wafanyabiashara kuelewa umuhimu wa kulipia Kodi kwa wakati wameweza kukusanya kiasi cha Tshs millioni 840.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika:
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda