Jumla ya Walimu 50 wanaofundisha somo la Hisabati kwa shule za msingi, kutoka Kata 19 zilizopo katika Halmashauri ya wilaya ya Bunda, siku ya tarehe 20/11/2023, walipatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo na mbinu ya kufundisha somo la Hisabati kwa wanafunzi wa shule za Msingi.
Mafunzo hayo yalitolewa na Wakufunzi kutoka chuo cha Ualimu Tarime ambao ni ndugu Ndulu Francis Nkenyenge na ndugu Zacharia Francis Muyembe. Walianza kwa kuwaambia walimu kuunda vikundi ambavyo watajadiliana kwa pamoja kwa kila kundi kuandika matarajio yao wanayotarajia kuyapata baada ya mafunzo hayo.
Mkufunzi Ndulu Francis Nkenyenge, aliwaambia malengo makuu ya mafunzo haya ni kuwawezesha walimu kuchanganua dhana mbalimbali za Hisabati na kuzihusianisha na maisha ya kila siku. Hivyo aliwaambia wawe wanatumia mifano halisi na sio kutoa mifano ambayo haipo katika jamii, yaani mifano ya kusadikika, wanatakiwa watumie mifano halisi ya vitu vinavowazunguka wanafunzi ili wawaelewe.
Ndugu, Nkenyenge pia, aliwaambia walimu wanatakiwa kufundisha kwa ufanisi na umahiri wenye changamoto kwa kutumia mbinu za ufundishaji na dhana stahiki. Pia, wanatakiwa kumudu stadi za upimaji endelevu ili kuboresha ufundishaji wa umahiri wenye changamoto katika ufundishaji.
Baada ya kuelezwa malengo ya mafunzo hayo, Mkufunzi Zacharia Francis Muyembe aliwafundisha umuhimu wa Mafunzo Endelevu Kazini (MEWAKA), kwa kuwataka kuyazingatia kwa umakini kwani yanasaidia kutatua changamoto za ujifunzaji na ufundishaji mahiri mbalimbali.
Alisema mafunzo hayo yanasaidia kuibua mbinu na njia za kufundishia katika mahiri mbalimbali, na pia yanasaidia kuboresha ufundishaji kwa kutumia dhana. Na yanasaidia kufanya tathimini baada ya upimaji, na yanamsaidia Mwalimu kumudu masomo mengine kwa kujifunza.
Kupitia mafunzo haya walimu waliweza kutambua umuhimu wa MEWAKA na fursa zake katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa Hisabati, pia waliweza kubainisha uhusiano wa kimaudhui kati ya moduli ya MEWAKA na muhtasari wa somo la Hisabati kwa darasa la Saba.
Walimu waliwashukuru Wakufunzi kwa mafunzo waliyowapa, pia waliwashukuru, SHULE BORA kwa kuwezesha kufanyika kwa mafunzo haya, na wameomba mafunzo haya yawe endelevu na sio kwa somo la Hisabati peke yake na masomo mengine.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0754335739
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda